Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Eleuther Mwageni amesema wanafunzi wenye vigezo vya kujiunga na elimu ya juu wanatakiwa kuripoti chuoni Oktoba 30 ili kuanza masomo yao.
Prof.Mwageni ameyasema hayo leo wakati anatoa ufafanuzi juu ya tarehe ya kufunguliwa kwa vyuo kutokana na mkanganyiko ambao wameupata baadhi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo kwa mwaka 2017/18.
Amesema,Tarehe ya Kalenda ya masomo haijabadilika ambayo ni Oktoba 30 nakwamba wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo ya elimu ya juu kwa mwaka huo.
Aidha Prof. Mwageni amesema zaidi ya wanafunzi laki nne na Elfu hamsini tayari wameshapata vyuo na kwamba kinachosubiriwa katika awamu ya tatu ni kupitisha wanafunzi wengine elfu kumi na mbili ili kufikia malengo ambayo ni wanafunzi elfu hamsini na saba.
Mapema mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alishauri TCU iweke utaratibu wa wanafunzi kuomba nafasi chuoni moja kwa moja ili waende vyuo wanavyotaka wao tofauti na awali ambapo zoezi la kupanga vyuo lilikuwa linasimamiwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini.