Bomu kubwa zaidi kuwahi kutengenezwa na Marekani na ambalo halitumii nyuklia limeangushwa kwenye milima ya Afghanistan na kuripotiwa kuwaua mamia ya wapiganaji wa kundi la Islamic State ambao wamekuwa wakijificha kwenye mahandaki.
Serikali ya Afghanistan imethibitisha kudondoshwa kwa bomu hilo, ambalo pamoja na nguvu kubwa ya uharibifu inayotokana na silaha hiyo, mamlaka nchini humo zimekanusha taarifa kuwa kuna raia wa kawaida waliouawa.
Bomu hilo aina ya GBU-43/B Massive Ordnance Air Blast, linafahamika kwa jina jingine kama “Mama wa mabomu yote” na limetumiwa kwa mara ya kwanza kulenga ngome za wapiganaji wa IS mashariki mwa jimbo la Nangarhar hapo jana jioni.
Bomu hili lilitarajiwa kumaliza kabisa uwezo wa kundi la Islamic State nchini Afghanistan na kutuma onyo kwa kundi la Taliban ambalo linajiandaa na mashambulizi yake ya mwaka.
Mlipuko wa bomu hilo ulisikika kwenye umbali mkubwa wa jimbo la Nangarhar na kusambaza moto kuharibu kile ambacho maofisa wa Afghanistan wanasema mtandao wa kundi la IS waliokuwa wakitumia mashimo kujificha.