Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na baiskeli, kuanzia leo wamepigwa marufuku kusafirisha mazao ya misitu kama vile mkaa na mbao kwa kutumia vyombo hivyo, na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria.

Imebainika kuwa kutokana na kukithiri kwa usafirishaji wa mazao hayo kwa vyombo hivyo vya usafirishaji, serikali hupoteza jumla ya fedha za maduhuli zinazokadiriwa kufikia Sh bilioni 1.1 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh bilioni 13 kwa mwaka.

Mkakati huo wa kuwakamata watakaokiuka agizo hilo, unatekelezwa na mamlaka tatu ambazo ni Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama wa Barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Na kwamba, atakayekamatwa na kubainika kuwa amesafirisha mazao hayo kwa kutumia vyombo hivyo vya usafiri atatozwa faini ya papo kwa hapo ya Sh 30,000, kifungo au vyote kwa pamoja.

Akizungumza Dar es Salaam , Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano TFS, Glory Mziray amesema Sheria na Kanuni za Sheria ya Misitu zinapiga marufuku mazao ya misitu kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na baiskeli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *